Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa pongezi kwa Timu ya Tanzania ya Wanawake ya Kriketi kwa kutwaa Ubingwa Juni 18, 2022 kwenye mashindano ya Kwibuka Cup nchini Rwanda, yaliyoshirikisha nchi nane( Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Botswana , Nigeria, Brazil na Ujerumani) bila kufungwa na timu yoyote.
Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa anaoutoa katika michezo.
Amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha michezo kwa kuweka mikakati kabambe chini ya uongozi wa Samia imeleta matokeo chanya kwenye sekta za michezo na sanaa hapa nchini.
Amesema taarifa ya hali ya uchumi wa nchi iliyosomwa bungeni hivi karibuni imeonesha kuwa sanaa na burudani zimechangia kwa asilimia 19.4 katika kipindi cha mwaka 2021 na kuziacha kwa mbali sekta mbalimbali.
Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuifanya michezo kuwa uchumi badala mazoe ya kuifanya michezo kama kitu cha burudani pekee.
Aidha, amesema Serikali tayari inazigharimia timu zote za taifa zinazojiandaa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kwa kuziweka kambini kuanzia mwanzo wa mwaka huu.
Hivi karibuni Mhe. Mchengerwa amekaririwa vyombo vya habari akisisitiza kuwa michezo na sanaa ni uchumi hivyo wanamichezo na wasanii wanapaswa kutambua kuwa vipaji walivyonavyo ni mtaji wa maisha yao.
Ujumbe wa Klabu ya Southampton uliokutana na Mhe. Waziri Mchengerwa na kufanya mazungumzo ya kuinua michezo ulioongozwa na Mkuu wa Idara ya Biashara ya klabu hiyo David Thomas pia ulimpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye michezo na kumzawadia jezi ambayo ilipokelewa kwa niaba yake na Mhe. Mchengerwa.